JE, UGONJWA WA KIFUA KIKUU HUSABABISHWA NA NINI?




Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea sana kwa watu masikini duniani (Disease of poverty). Magonjwa mengine katika jamii ya disease of poverty ni malaria na Ukimwi (AIDS).
Ugonjwa wa kifua kikuu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea, ukimwi asilimia 95 na malaria asilimia 90.
Magonjwa haya matatu husababisha vifo asilimia 10 ya idadi ya watu wote duniani kwa ujumla, ambapo inakisiwa watu wote duniani ni 6.91 bilioni kulingana na kituo cha kuhesabu watu cha Marekani ( US Census Bureau).














Kwa Tanzania, watu 120,191 hukisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka, hii ni kutokana na taarifa ya shirika la USAID ya mwaka 2007. Kati ya watu hawa
(120,191), 56,233 ni wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huu kupitia makohozi yaani sputum smear positive (SS). Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka nchini Tanzania.
Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu. Kati ya asilimia 50 ya wagonjwa wa kifua kikuu waliopimwa virusi vya ukimwi mwaka 2007, inakadiriwa ugonjwa wa ukimwi huathiri asilimia 47 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu.
Ugonjwa sugu wa kifua kikuu (Multidrug resistant tuberculosis) huathiri watu 1,300 nchini Tanzania kulingana na taarifa ya mwaka 2007.
Je, ugonjwa wa kifua kikuu husababishwa na nini?
Ugonjwa wa kifua kikuu, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis. Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ngombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na kadhalika.

Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.

Mycobacteria bovis ambayo huathiri ngombe, inaweza kuambukiza binadamu kama atakula bidhaa zinazotokana na maziwa ya ngombe ambayo yameathirika na bakteria hawa kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream nk. Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.

Ni asilimia 10 tu ya watu walio na bakteria wa Mycobacteria tuberculosis ambao hawapati ugonjwa huu wa kifua kikuu.
Mycobacteria tuberculosis waligundulika kwa mara ya kwanza na mwanasayansi kutoka ujerumani anayeitwa Robert Koch mwaka 1882 na kupewa tuzo ya amani ya Nobel kwa ugunduzi wake huu.

Kuna aina ngapi za ugonjwa wa kifua kikuu?
Kuna aina kuu tatu za ugonjwa wa kifua kikuu;
  • Kifua kikuu kinachosababisha madhara (Active tuberculosis) – Hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa bakteria wasisababishe madhara. Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yoyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu.
  • Ugonjwa usiosababisha madhara(Inactive tuberculosis) – Kwa kitaalamu pia unaitwa latent TB. Hapa inaamaanisha ya kwamba kinga ya mwili imeweza kuwadhibiti bakteria na kuwafanya kushindwa kusababisha madhara. Mtu mwenye latent TB, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu. Aina hii inaweza kujirudia baadae na kuathri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadae huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.
  • Ugonjwa uliosambaa Mwilini (Milliary tuberculosis) – Hii hutokea pale ambapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo (pericadium), mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system. Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.
 
Vihatarishi vya ugonjwa wa kifua kikuu
Vihatarishi vya ugonjwa huu ni kama ifuatavyo;
  • Kuzeeka
  • Unywaji pombe kupindukia
  • Kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi nk.
  • Magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari nk.
  • Wafanyakazi wa huduma ya afya
  • Ugonjwa wa HIV
  • Utapia mlo
  • Umaskini au hali duni ya kipato
  • Kuishi kwenye nyumba za jamii mfano nyumba za wazee
  • Wale wasio na makazi
  • Baadhi ya dawa – Dawa za ugonjwa wa maumivu ya mifupa (athritis)
  • Wasafiri au watalii kutoka nchi zilizo na idadi kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu.
  •  
Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu
  • Kukohoa zaidi ya wiki 2-3 na kuongezeka kutoa makohozi
  • Kukohoa damu
  • Homa
  • Kupungua hamu ya kula
  • Kupungua uzito kwa asilimia 10 ya mwili.
  • Kutokwa na jasho kwa wingi wakati wa usiku
  • Uchovu
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Maumivu ya kifua
  • Kupumua kwa shida
Vipimo vya kifua kikuu
  • Kipimo cha makohozi(Sputum for AFB) – Makohozi huchukuliwa kwa siku tatu mfululizo muda wa asubuhi na kupelekwa maabara kufanyiwa uchunguzi ili kuweza kugundua kama mtu ana TB. Kwa wale wagonjwa wasioweza kutoa makohozi au wale wenye TB ya tumbo basi hufanyiwa kipimo cha gastric lavage.
  • Picha ya X-ray ya kifua – TB ya mapafu huweza kugundulika kutumia kipimo hiki.
 
  • Kipimo cha kwenye ngozi – Tuberculin skin test (Mantoux test) – Hufanywa na daktari. Daktari huchoma dawa ya protein purified derivatives (PPD) kwenye ngozi ya mgonjwa, kama kutatokea uvimbe zaidi ya 5mm (0.2 in) baada ya masaa 48, basi mgonjwa huyo ana TB. Kipimo hiki kinaweza kutoa majibu ambayo si sahihi hasa kwa wale ambao wamepata chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu, wenye ugonjwa wa hodgkins lymphoma, sarcoidosis na hata utapia mlo. Majibu yake ni lazima yasomwe na daktari.
  • Kipimo cha PCR (Polymerase Chain Reaction assay) – Kipimo hiki kinahusisha utambuzi wa bakteria wanaosababisha kifua kikuu kupitia vina saba vyao (DNA of bacteria). Ni kipimo cha uhakika zaidi.
  • Kuotesha bakteria maabara (Bacteria culture) – Kipimo hiki huchukua muda mrefu na ni ghali.
Tiba ya kifua kikuu
Tiba ya kifua kikuu inahusiha matumizi ya dawa za kifua kikuu kwa muda wa miezi sita au tisa. Dawa hizi zinahusisha matumizi ya miezi 2 ya kwanza ya dawa aina ya isoniazid, rifampicin, pyrazinamide, na matumizi ya miezi 4 ya isoniazid, rifampicin na ethambutol au streptomycin. Dawa hizi hutolewa chini ya uangalizi yaani mgonjwa anakunywa chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya (Directly ObserveTreatment, short course). Tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu inatolewa bure nchini kote Tanzania.
Upasuaji unaweza kufanyika kwenye mapafu kama dawa zimeshindwa kutibu kifua kikuu.
ya kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu
 
  • Chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu ipo na inasaidia kukinga TB (BCG Vaccine) na imeleta mafinikio katika kukabiliana na kifua kikuu. Kawaida hutolewa kwa watoto baada ya kuzaliwa.
  • Kuziba pua na mdomo kwa kitambaa (mask) ili kujikinga na kifua kikuu. 
  •  
  •  
  • Kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha kinga ya mwili.
  • Kupata usingizi wa kutosha.
  • Kwenda hospitali kufanya vipimo mara kwa mara. Inashauriwa kufanya kipimo cha ngozi angalau mara moja kwa mwaka.
  • Kuimarisha kinga ya mwili kwa kula vyakula venye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora.
  • Kutumia dawa aina ya isoniazid (INH) kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa kifua kikuu.
  • Shirika la afya duniani (WHO) linapendekeza wagonjwa wa ukimwi (HIV) ambao wana Latent TB wapewe dawa ya isoniazid (INH) kama kinga dhidhi ya kifua kikuu kila inapohitajika.
  •  
  • Kuepuka mikusanyiko au mrundikano wa watu kama vile kwenye mabweni, kambi za jeshi, baa nk
  • Kuishi kwenye nyumba ambayo ina mfumo mzuri wa kuingiza na kutoa hewa yaani iwe na madirisha makubwa na ya kutosha.

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZIPATIKANAZO KWA KUTUMIA TUNGUJA PORI,NYANYA ZA MSHUMAA/CHUNGU/NGOGWE KIAFYA.

FAIDA YA MBOGA YA MCHICHA NI DAWA YA KUTIBU MARADHI MENGI TU UKITUMIA.

DALILI YA KUZIDI ASIDI MWILINI YOUR BODY IS ACIDIC HERE IS WHAT YOU NEED TO DO (THE REAL TRUTH BEHIND CANCER)