Glakoma Ugonjwa Unaosababisha Upofu
Glakoma Ugonjwa Unaosababisha Upofu
TAZAMA neno la mwisho la sentensi hii kwa muda fulani. Bila kusogeza macho yako, je, unaweza kuona sehemu fulani ya juu, ya chini, na kandokando ya gazeti hili? Yaelekea unaweza kwa sababu jicho lina uwezo wa kuona vitu vilivyo kandokando huku ukitazama mbele. Uwezo huo wa jicho hukuwezesha kutambua kwamba kuna mtu anayekukaribia kutoka kando. Hukusaidia usikanyage vitu vilivyo chini na kuepuka kujigonga ukutani unapotembea. Hata unapoendesha gari, uwezo huo wa jicho unaweza kukusaidia kujua kwamba mtu fulani anayetembea ameingia barabarani.
Lakini hata sasa unaposoma habari hii, huenda uwezo wa jicho lako wa kuona vitu vilivyo kando yako unadhoofika polepole bila wewe kujua. Inakadiriwa kwamba watu milioni 66 ulimwenguni pote wana magonjwa fulani ya macho ambayo kwa jumla huitwa glakoma. Zaidi ya watu milioni tano kati yao wamekuwa vipofu kabisa. Hivyo, glakoma ndicho kisababishi cha tatu kikuu cha upofu. Jarida la kitiba The Lancet linasema hivi: “Lakini, hata katika nchi zilizoendelea ambazo zina miradi ya kuelimisha jamii kuhusu glakoma, nusu ya watu walio na ugonjwa huo hawajui kwamba wanaugua.”
Ni nani wanaoweza kuugua glakoma? Ni njia zipi zinazotumiwa kuutambua na kuutibu?
Glakoma Ni Nini?
Kwanza, tunapaswa kufahamu mambo fulani kuhusu macho yetu. Kijitabu kilichochapishwa na Taasisi ya Glakoma ya Australia kinasema hivi: “Umbo la jicho hutegemea shinikizo, yaani, tishu laini za jicho hufurishwa kama tairi ya gari au puto.” Jicho lina misuli ya siliari ambayo husukuma umajimaji unaoitwa ute-maji kutoka kwenye mishipa ya damu na kuuingiza kwenye jicho. “Umajimaji huo huenea ndani ya jicho na kulowesha sehemu zake, kisha unarudi kwenye mfumo wa damu kupitia mirija midogo iliyo mbele ya jicho.”
Mirija hiyo ikiziba au ikisongamana kwa sababu yoyote ile, shinikizo ndani ya jicho huongezeka na hatimaye huanza kuharibu nyuzinyuzi za neva ambazo ziko nyuma ya jicho. Hali hiyo, inayoitwa glakoma ya open-angle, hupata asilimia 90 hivi ya watu wanaougua glakoma.
Shinikizo ndani ya jicho linaweza kubadilika mara nyingi kwa siku ikitegemea mambo mbalimbali kama vile mpigo wa moyo, kiasi cha vinywaji unavyokunywa, na mkao wa mwili. Mabadiliko hayo ya kawaida hayaharibu jicho. Shinikizo kubwa kwenye jicho halionyeshi kwamba mtu ana glakoma kwani shinikizo la macho ya watu hutofautiana. Hata hivyo, shinikizo kubwa ni dalili moja ya ugonjwa wa glakoma.
Aina nyingine ya glakoma (acute, au angle-closure glaucoma) ambayo hutokea mara chache hufanya nafasi iliyo kati ya konea na irisi kuwa ndogo sana isivyo kawaida. Tofauti na glakoma ya open-angle, shinikizo la jicho huongezeka ghafula katika aina hii ya glakoma. Hiyo husababisha maumivu makali jichoni, kutoona vizuri, na kutapika. Mara nyingi hali hiyo husababisha upofu mtu asipotibiwa saa chache tu baada ya kupata dalili hizo. Kuna aina fulani ya glakoma (secondary glaucoma) inayosababishwa na hali nyingine kama vile uvimbe, mtoto wa jicho (cataract), au majeraha ya macho. Vilevile watu wachache hupata aina ya nne ya glakoma (congenital glaucoma). Aina hiyo ya glakoma huanza mtoto anapozaliwa au muda mfupi baadaye, nayo hutambuliwa ikiwa mtoto ana mboni kubwa sana na anaathiriwa sana na mwangaza.
Jinsi Glakoma Husababisha Upofu
Ugonjwa wa glakoma unaweza kusababisha jicho moja lipoteze asilimia 90 ya uwezo wa kuona bila wewe kujua. Inawezekanaje? Kila mtu ana sehemu ndogo ya mviringo nyuma ya kila jicho. Sehemu hiyo iliyo kwenye retina, ambako nyuzi za neva huungana ili kufanyiza neva ya jicho, haina chembe za kupokea mwangaza. Hata hivyo, hatutambui kwamba tuna sehemu hiyo katika jicho kwa sababu ubongo una uwezo wa kukamilisha picha ya vitu tunavyoona. Ni ajabu kwamba uwezo huo wa ubongo ndio unaofanya ugonjwa wa glakoma kutokea polepole na kuwa hatari sana.
Dakt. Ivan Goldberg, ambaye ni mtaalamu maarufu wa macho huko Australia, aliliambia Amkeni! hivi: “Glakoma huonwa kuwa mwizi anayenyemelea kwa sababu haimwonyeshi mtu kwamba anaugua. Aina fulani ya glakoma ambayo huwapata watu wengi zaidi huanza polepole, nayo huendelea na kuharibu sehemu ya neva inayounganisha jicho na ubongo bila kuonyesha dalili zozote. Iwe macho yako hutokwa au hayatokwi na machozi, yawe makavu au si makavu, yawe yanaona vizuri au hayaoni vizuri unaposoma na kuandika, bado unaweza kuwa na ugonjwa wa glakoma. Huenda ukawa unaugua glakoma sana hata ikiwa huhisi tatizo lolote kwenye macho.”
Kutambua Glakoma
Kwa kusikitisha, hakuna njia hususa ya kuonyesha ikiwa mtu ana ugonjwa huo. Kwa kutumia kifaa fulani, daktari wa macho anaweza kuanza kukuchunguza kwa kupima shinikizo la umajimaji ndani ya macho yako. Kifaa hicho hutumiwa kubonyeza konea, au sehemu ya mbele ya jicho. Nguvu inayotumiwa kubonyeza konea hupimwa, na kwa njia hiyo shinikizo la jicho lako hujulikana. Pia kwa kutumia vifaa vingine, daktari wa macho anaweza kuchunguza ikiwa kuna chembe zilizoharibika kwenye sehemu ya neva inayounganisha jicho na ubongo ili kuona kama una dalili za glakoma. Dakt. Goldberg anasema: “Sisi huchunguza iwapo nyuzi za neva au mishipa ya damu iliyo nyuma ya jicho ina umbo lisilo la kawaida, kwani hiyo ni dalili ya kuonyesha kwamba neva zinaharibika.”
Njia nyingine ya kuchunguza glakoma inahusisha kutambua eneo lote ambalo jicho la mtu linaweza kuona anapotazama sehemu moja. Dakt. Goldberg anaeleza hivi: “Mtu anayechunguzwa hutazama ndani ya bakuli lenye mwangaza mweupe, kisha mwangaza mwingine mdogo mweupe unaong’aa zaidi hutokezwa kwenye bakuli hiyo. Mtu huyo anapoona mwangaza huo mdogo mweupe, yeye hubonyeza kidude fulani.” Ikiwa mtu haoni mwangaza huo wakati unapokuwa kandokando, basi huenda ana glakoma. Vifaa vipya vinaundwa ili kurahisisha mbinu hizo za uchunguzi.
Ni Nani Wanaoweza Kupata Glakoma?
Paul ni mwanamume mwenye afya nzuri aliye na umri wa miaka 40 na kitu. Anasema: “Nilienda kuchunguzwa na mpimaji wa macho ili nipate miwani mipya, naye akaniuliza ikiwa kuna mtu anayeugua glakoma katika familia yetu. Nilifanya uchunguzi na kugundua kwamba shangazi yangu na mjomba wangu waliugua ugonjwa huo. Alipendekeza nichunguzwe na mtaalamu wa macho. Mtaalamu huyo aligundua kwamba ninaugua glakoma.” Dakt. Goldberg anaeleza hivi: “Ikiwa baba yako au mama yako ana ugonjwa huo, basi uwezekano wa kuupata ni mara tatu hadi tano zaidi. Na ikiwa ndugu yako au dada yako ana glakoma, uwezekano wa kuupata ni mara tano hadi saba zaidi.”
Akionyesha mambo mengine yanayosababisha ugonjwa huo, Dakt. Kevin Greenidge, wa Taasisi ya Glakoma ya Marekani, alisema hivi: “Unahitaji kuchunguzwa macho kila mwaka ikiwa umepita umri wa miaka 45 na una asili ya Kiafrika, au ikiwa mojawapo ya hali zifuatazo zinakuhusu—mtu fulani katika familia yenu amewahi kuugua glakoma, una matatizo ya kutoona mbali, una ugonjwa wa kisukari, umewahi kujeruhiwa macho, au unatumia kwa ukawaida dawa aina ya cortisone au steroid.” Hata ikiwa mtu hajafikisha umri wa miaka 45 na hajawahi kupatwa na hali hizo zilizotajwa, taasisi hiyo inapendekeza apimwe macho baada ya kila miaka minne ili ionekane kama ana glakoma. Ikiwa umepita umri wa miaka 45, unahitaji kupimwa macho baada ya kila miaka miwili.
Kutibu na Kuzuia Glakoma
Paul hutibiwa glakoma kwa kutia dawa ya matone kwenye macho. Paul anasema hivi: “Dawa ninayotumia hupunguza ute-maji katika mboni.” Isitoshe, kwa kutumia mwangaza fulani, Paul alitobolewa vishimo vidogo katika sehemu ya mbele ya jicho karibu na mahali mashimo ya kawaida ya kuondolea ute huo hupatikana. Anasema hivi: “Niliogopa sana jicho langu lilipotibiwa mara ya kwanza kwa kutumia mbinu hiyo, na hilo lilinifanya niumie zaidi. Hata hivyo, nilipotibiwa jicho la pili siku chache baadaye, sikuwa na wasiwasi kwani nilijua yale nitakayokabili. Nilikuwa mtulivu sana hivi kwamba nilidhania kuwa daktari amenitibu haraka sana.” Matibabu hayo yamesaidia kusawazisha shinikizo la macho ya Paul.
Paul ana maoni mazuri. Anasema hivi: “Retina za macho yangu zimeathiriwa kidogo tu, nami nashukuru kwamba bado naweza kuona vizuri hata vitu vilivyo kandokando. Ikiwa nitaendelea kutumia dawa kila siku, yaelekea nitaendelea kuona.”
Je, ugonjwa wa glakoma umeanza kukuathiri polepole? Iwapo hujawahi kupimwa glakoma, na hasa ikiwa uko miongoni mwa watu wanaokabili hatari ya kuupata, itafaa uende kuchunguzwa na daktari. Dakt. Goldberg anasema kwamba “madhara mengi yanayosababishwa na glakoma yanaweza kuzuiwa kwa kupata matibabu mazuri mapema.” Naam, unaweza kuzuia na kutibu ugonjwa huo unaosababisha upofu!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Unakabili hatari kubwa ya kupata glakoma ikiwa
● Una asili ya Kiafrika
● Mtu fulani katika familia yenu ana glakoma
● Unaugua kisukari
● Huwezi kuona vitu vilivyo mbali
● Umetumia kwa muda mrefu dawa aina ya cortisone au steroid inayotumiwa katika dawa za kujipaka na dawa za pumu za kujipulizia
● Umewahi kujeruhiwa jicho
● Una zaidi ya miaka 45
[Picha]
Kuchunguzwa kwa ukawaida kunaweza kuzuia upofu
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
GLAKOMA YA OPEN-ANGLE
Konea
Irisi
Lenzi
Retina
Sehemu ya mviringo nyuma ya jicho; hapa ndipo nyuzi za neva huungana ili kufanyiza neva ya jicho
Neva ya jicho hupeleka picha kwenye ubongo
Misuli ya siliari, mahali ambapo umajimaji huo hutengenezwa
1 Ute-maji ni umajimaji unaolowesha lenzi ya jicho, irisi, na sehemu ya ndani ya konea. Ute-maji si machozi, ambayo husafisha sehemu ya nje ya jicho
2 Mirija iliyo katika sehemu ya mbele ya jicho huondoa umajimaji huo
3 Mirija hiyo ikiziba au kubanwa, shinikizo ndani ya jicho huongezeka
4 Shinikizo la jicho likiongezeka, nyuzinyuzi nyeti za neva zilizo nyuma ya jicho huharibika na kusababisha glakoma au kupunguza uwezo wa kuona
[Picha katika ukurasa wa 25]
Sehemu ya mviringo nyuma ya jicho
Unachoweza kuona
JICHO LINALOONA VIZURI
HATUA ZA KWANZA ZA GLAKOMA
GLAKOMA ILIYOZIDI
[Hisani]
Photos of optic disks: Courtesy Atlas of Ophthalmology
Comments
Post a Comment