KUISHI UKWELI  WA MWALIMU

LICHA ya Mwasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kuwaacha Watanzania kwa takribani miongo miwili, maono yake mengi yanaendelea kuishi na kudumishwa na awamu ya tano.

Hivyo hata kama Mwalimu angefufuka leo, akifurahia muendelezo wa maono yake na mafanikio makubwa yaliyofikiwa.

Katika kumkumbuka Mwalimu. Nipashe, inazungumza na Mchumi na Mchambuzi wa masuala ya kijamii na maendeleo , Dk. Hoseana Lunogelo, kuangalia jinsi kazi za Mwalimu zinavyoakisiwa katika serikali  ya awamu  ya tano.

Anaanza kwa kutaja baadhi ya mambo akisema mojawapo ya  kitu ambacho Nyerere alikiota ni suala la kila Mtanzania kupata elimu ili kufuta ujinga , kujiepusha na maradhi na kujiondoa kwenye umaskini.

Anasema maono ya Mwalimu ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu yameendelea kuishi tena kwa kurejea sera ya elimu ya bure.

Nyerere akiiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1961 hadi 1985, alisimamia sera ya kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania ili kila mmoja  asome.

 Kwa kutumia rasilimali za umma alitoa kila kitu kuanzia vitabu, daftari , kalamu na mahitaji yote ya msingi.

Hata hivyo, Dk. Lunogelo anasema katika utekelezaji wa sera hiyo mambo mengi yalikwamia mikononi mwake kwani shule hazikutosheleza, walimu , vifaa vya kufundishia na hata mahitaji mengine yalikosekana.

Hata hivyo, anasema awamu ya tano, imeitazama tena  azma ya sera la elimu bure kwa kuhakikisha kuwa elimu ni haki ya kila Mtanzania na inaanza tena kutolewa bure ili asitokee mtu anayeshindwa kusoma kisa ni maskini au hakuna shule.

Awamu ya tano kuanzia mwaka 2016  imeanza kutekeleza sera ya elimu bure ambayo inagharamiwa na serikali kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, anasema.

Licha ya kwamba Mwalimu alikuwa ametoa elimu bure hadi vyuo vikuu, alijua kuwa anaongoza taifa la watu maskini lakini wenye shauku ya kuboresha maisha yao.

Kwa kutembea ndani ya maono makubwa ya Mwalimu Nyerere, awamu ya tano imeweka mkazo kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa darasa la awali hadi sekondari.

Ni wazi uandikishwaji wa wanafunzi shuleni umeongezeka. Watoto wengi wanasoma na kufika kidato cha nne , kama isingekuwa hivyo huenda  wengi wangekosa nafasi kwa kuwa wazazi na walezi wangeshindwa kumudu gharama za kulipa ada na michango ambayo ni mzigo kwao.Anasema hili ni jambo ambalo lingemfurahisha Mwalimu Nyerere, iwapo angepewa nafasi ya kurudi na kuitazama tena Tanzania.

KUSAFISHA SERIKALI

Dokta Lunogelo anaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuonyesha ujasiri ambao Mwalimu Nyerere alikuwa anatamani kuuona katika viongozi wa Tanzania. Ujasiri huo ndiyo unaotumiwa kwenye kutumbua na kusafisha uongozi wa serikali ikibidi hata kufikisha mahakamani watuhumiwa ambao wamefisidi na kuhujumu nchi.

 Anauleleza kuwa ujasiri huo umekuwa ni dawa ya kupambana na kutokuwajibika ndani ya serikali, kutokana na kukithiri mdororo wa kiuongozi ambao uliwakera mno Watanzania kwa awamu zilizokuja baada ya Nyerere.

“Kilifika kipindi wananchi walitaka na kutamani mabadiliko. Hili lilitokana na kukithiri rushwa, ufisadi, ukosefu wa uwajibika na ubadhirifu mkubwa wa mali ya umma usiokemewa wala watuhumiwa kuwajibika.” Anakumbusha Dk. Lunogelo.

“Wananchi walichoshwa na maovu yaliyodumu ndani ya serikali tangu Mwalimu alipoacha kuiongoza serikali. Lakini awamu ya leo inakemea uovu na kuadhibu watuhumiwa. Kwa mfano inakemea ufisadi na imeanzisha kitengo katika Mahakama Kuu cha kushughulikia rushwa na uhujumu uchumi, “anasema.

Anadhani hiki ni kitu ambacho hata Mwalimu japo alitamani kufanya hivyo lakini hakuweza kutokana na pengine uvumilivu ambao alikuwa nao kwa baadhi ya watendaji akiamini kuwa hakuwa na wataalamu na pia walikuwa ndiyo wadau katika kupigania uhuru.

“Awamu ya Mwalimu ilikuwa inawajibisha kwa utaratibu wa kumwondoa mhusika anayetuhumiwa kuharibu sehemu moja. Lakini kilichotokea alihamishwa na kupelekwa kwenye shirika au kampuni nyingine ambako aliendelea kuvuruga.” Wakati huu hilo limedhibitiwa kama hutimizi wajibu wa kuwatumikia Watanzania awamu ya tano haikuvumilii.” Anasema.

HAKUNA KULEANA

Nyerere anapokumbukwa leo kuna baadhi ya Watanzania wanaomkosoa kwa kile Dk. Lunogelo anachokiita kuwa ni kuachia ‘uwepo donda ndugu’ la kutokuwajibishana  hasa kwa viongozi ambao waliyavuruga mashirika na kampuni za umma.

Wapo baadhi ya watendaji ambao ni wahusika kwenye masuala yaliyorudisha nyuma maendeleo. Leo wasingekuwa na nafasi kwa kuwa awamu ya tano imeondolewa utamaduni wa  kuleana.

“Mwalimu angeyashuhudia haya leo ya kuwajibishana angeisifu awamu ya tano kuwa imekuwa na ujasiri wa kipekee ambao hata yeye hakuuweza.” Anasema.  

KUIMARISHA CHAMA

Chama Cha Mapinduzi cha leo si legelege tena kama kile ambacho Mwalimi alikiacha, anaeleza mchumi huyu mbobezi.

Anasema , wakati Mwalimu akiwa Mwenyekiti na mkuu wa CCM, kulikuwa na upole  ndani ya chama na malalamiko, shutuma na ukosefu wa nidhamu. Hata hivyo, zama hizi ni CCM thabiti, inayojitegemea na ambayo inasimamia, kujikosoa na kujiimarisha ili  kujiondoa  na kujinasua na  utegemezi wa fedha za kuombaomba.

Chama Nyerere alikiacha na mali za milioni na mtaji mkubwa kuanzia wanachama na umma unaokiunga mkono , lakini hakikuwa na uongozi thabati kama ulivyo sasa ambao unafukuza wananchama wasiowaadilifu na kukemea kila aina ya hujuma inayofanyika ndani ya chama, anachambua mchambuzi huyo.

Maelezo hayo ya Dk. Lunogelo yanaakisiwa na kauli anazotoa Dk. Bashiru Ally, akisema kuna wizi ndani ya CCM unaofanywa na watu wenye majina makubwa na kwamba iwapo ataamua kutaja majina yao, umma utashangaa na kushindwa kuamini.Akizungumza katika mdahalo wa Kumbukumbu ya Miaka 19 ya Mwalimu Nyerere,anataja moja kwa moja kuwa kuna wezi wanaojifanya wazalendo, wamepora ardhi, wameiba magari na mali za chama, hata hivyo wanapozungumza majukwaani wananchi wanaweza kuwaamini na kudhani kweli ni  wazalendo.

Pamoja na kukimulika chama na uongozi wake , kumekuwa na ujasiri wa hali ya juu, kuacha kuogopana na kuchukua hatua mambo yanayofanywa na awamu ya tano, ambayo ni marekebisho yanayoleta mwanga mpya ndani ya chama kinachoiongoza serikali.

KUISHI UKWELI  WA MWALIMU

Dokta Lunogelo anasema katika mambo ambayo yamempandisha chati na kumuenzi Mwalimu Nyerere,yanayofanywa na awamu hii ni kuishi ukweli aliokuwa anauzungumza na kuutamani uwepo siku zote.

Anarejea kitabu cha Mwalimu cha ‘Tujisahihishe’akisema: “Katika andiko hili anazungumzia ukweli na jinsi ambavyo ni muhimu katika maisha ya Watanzania.

Anamnukuu Mwalimu aliyesema: Ukweli una tabia moja nzuri sana. Ukweli haujali mdogo wala mkubwa, haujali mrefu wala mfupi, haujali mwenye cheo au asiye na cheo, haujali mzee au mtoto.” Anakumbusha, kuwa katika kufafanua dhana ya ukweli Mwalimu anataja  mfano kuwa iwapo wewe ni mzee mzima na ukaona jiwe la mviringo ukadhania ni mpira.

 Baada ya hapo unajitayarisha kupiga teke akidhania ni mpira  lakini mtoto mdogo akakushauri usipige kwani ni jiwe la mviringo lakini , mzee akampuuza kwa vile ni mtoto akiamini kuwa hawezi kumwambia kitu na akapiga jiwe hilo teke , Mwalimu anawahakikishia wasomaji kuwa   hakika dole gumba litavunjika na mzee atakuwa anachechemea kwa kupuuza ukweli.

 Anaonya kuwa watu wasidharau ukweli kwani daima unabaki kama ulivyo.

“Hili la kusimamia ukweli ndilo linalofanyika na serikali ya awamu ya tano. Hakuna kupuuza ukweli. Awamu ya tano haina unafiki kila jambo linaelezwa kwa usahihi na ukweli unajulikana.  Serikali ya sasa inasimamia ukweli na hili limesaidia kuibua masuala yaliyokuwa yamefichika kwa mfano mikataba ya madini isiyonufaisha taifa, masuala ya usafirishaji wa makinikia bila kukaguliwa na kudhibitiwa.  

Anasema kila anayekosea serikali haina kigugumizi awe mkubwa, mtoto, tajiri, mwekezaji wa kigeni, mkurugenzi, kiongozi   au mzee anaelezwa ukweli na ubakia kuwa hivyo daima.

“Haya ndiyo ambayo Nyerere aliyoyataka na aliyoyaandikia katika kitabu cha Tujisahihishe. Na hayo ndiyo awamu ya tano inayoyaishi falsafa ya Mwalimu ya kuheshimu ukweli.” Anasem Lunogelo.

Falsafa hii ya Mwalimu ilikuwa inalenga kutaka watu wasiogope kuwaambia wengine ukweli ili jamii, taifa na dunia viwe na amani na watu waishi kwa furaha.

Katika miaka mingine mingi zaidi ya kumkumbuka na kuheshimu kazi zilizotukuka alizofanya Mwalimu watu wasipuuze ukweli.

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZIPATIKANAZO KWA KUTUMIA TUNGUJA PORI,NYANYA ZA MSHUMAA/CHUNGU/NGOGWE KIAFYA.

FAIDA YA MBOGA YA MCHICHA NI DAWA YA KUTIBU MARADHI MENGI TU UKITUMIA.

DALILI YA KUZIDI ASIDI MWILINI YOUR BODY IS ACIDIC HERE IS WHAT YOU NEED TO DO (THE REAL TRUTH BEHIND CANCER)