Je utamaduni wa kujenga nyumba za nyasi unatokomea Kenya?
Ni majira ya mvua ya masika katika maeneo mbali mbali nchini Kenya na kwa kawaida wakenya wengi huzingatia mvua kuwa Baraka. Lakini mwaka huu mvua imekuja na kero la mafuriko.
Maeneo mengi ya Kenya na hasa katika mji mkuu Nairobi pamoja na viunga vyake yameshuhudia mafuriko ambayo yamesababisha vifo pamoja na uharibifu wa mali.
Lakini katika kijiji cha Chesamis, yapata kilomita 500 magharibi mwa mji mkuu Nairobi, mvua ya masika huleta masaibu kwa Bi. Emilly Chemto Boiyo mama mjane aliye na watoto sita.
Katika boma lake ana nyumba moja tu ya mviringo iliyojengwa kitamaduni kwa kuezekwa nyasi. Chumba chenyewe ni mviringo wenye upana kama futi sita hivi.
Ananitembeza ndani ya chumba hiki kido na dalili ya uchochole inajitokeza. Katika pembe moja ananionyesha sehemu anayotumia kama jikoni.
- Serikali Tanzania yamuonya Diamond Platnumz
- Trump atarajiwa kutangaza vikwazo dhidi ya China
- Mark Zuckerberg aomba radhi kwa kashfa ya Analytica
'' hapa ndio jiko la kupikia. Na hapa ndio pahali pa kulala,'' anasema.
Ni vigumu kuamini kwamba yeye pamoja na wanawe sita wanalala katika chumba hiki.
''tunajibana sote papa hapa hadi tunatoshea''
Anasema inabidi kila siku shughuli za kupika zinafanywa mapema ili kuepuka bughudha ya moshi mkali unaotokana na kuni wakati wa kulala.
Paa ya chumba hiki kidogo cha Bi. Emilly Chemto Boiyo linavuja wakati wa mvua. Inambidi yeye na watoto wake kusimama katika sehemu moja ya chumba hiki ili kuepuka kulowa maji ya mvua.
Lakini sasa kundi la mafundi wa ujenzi limewasili pamoja na mabati, misumari na miti ya ujenzi. Bi Emilly Chemto ni mmoja wa wakaazi wengi wa eneo bunge la Kimilili Magharibi mwa Kenya ambao wamenufaika na mradi wa kubomoa nyumba zilizoezekwa kwa nyasi na kujenga zile zilizoezekwa kwa mabati. Ni mradi uliopewa jina la 'ondoa nyasi kimilili' na mbunge wa eneo hili Didmus Barasa.
Leo bwana Barasa mwenyewe anaongoza shughuli za ufundi. Anapanda mwenyewe juu ya paa la chumba kipya kinachojengwa na kuezeka mabati.
Kila anapogonga msumari, wanaume kwa wanawake, wazee kwa vijana waliokusanyika kushuhudia mbunge wao akijengea mmoja wao nyumba wanashangilia kwa nyimbo.
'Nafikiri jambo la muhimu kwangu mimi kama kiongozi ni kuhakikisha kwamba yale mahitaji matatu muhimu kwa binadamu yaani makaazi mazuri, elimu na afya yanatiliwa maanani.
Nilipozungumza na wananchi wangu jambo la kwanza walilonieleza ni kwamba ingekuwa bora nianze kwa kuhakikisha kwamba wanakuwa na makaazi yaliyo afadhali,'' anasema Bwana Barasa.
Anasema kuna umaskini mkubwa sana katika eneo bunge lake na wengi wa raia wa Kenya hawana uwezo wa kumudu gharama ya vifaa vya ujenzi wa nyumba za kisasa.
''Nadhani bado kuna pengo kubwa sana kati ya watu matajiri na watu maskini Kenya''
''wanaoumia sana katika hali hii ni wanawake na watoto''
Anasema wanaume wengi wametorekea mijini kutafuta ajira ingawa ajira yenyewe wanayoipata haiwezi kukidhi mahitaji ya familia zao nyumbani.
Bila msaada familia kama hizi hukumbwa na mateso makubwa.
Lengo la mradi huu ni kuhakikisha kuwa nyumba zote zilizoekwa kwa nyasi katika eneo bunge lake zinabomolewa na kujengwa zile zilizoezekwa kwa mabati.
Na alipoulizwa kuhusu kutoweka kwa utamaduni endapo nyumba zote za nyasi zitatoweka, bwana Barasa anasema hata bila kuzibomoa nyumba hizo bado zitatoweka tu kwa sababu ni vigumu nyasi ya kuezeka kupatikana siku hizi kutokana na uhaba mkubwa wa ardhi ambao unayakumba maeneo mengi ya Kenya.
Ni wazo ambalo analiunga mkono bwana Muliro Telewa ambaye aliwahi kuwa mwandishi wa BBC na sasa amestaafu.
Katika kijiji chake cha Kona Mbaya, yapata kilomita 50 kutoka katika mji wa kilimo wa Kitale, bwana Telewa ni mmoja wa watu wachache katika eneo la magharibi mwa Kenya ambao wanaendeleza utamaduni wa kujenga nyumba zilizoezekwa kwa mabati.
Licha ya uhaba wa nyasi anazidi kujitahidi kujenga vyumba zilizoezekwa kwa nyasi mbali na nyumba za kisasa zilizoekwa kwa mabati katika boma lake.
Leo Bw. na Bi Horst Stadler ambao ni wazee waliostaafu kutoka Austria wamemtembelea bwana Telewa. Wao huzuru Kenya kila baada ya miaka minne na mbali na kutalii maeneo mbali mbali ya Kenya wanapenda kuja kwa Telewa kubarizi katika vyumba hizi za nyasi.
Wanasema wakija Kenya wanapenda kuishi maisha ya kitamaduni. Wanasema nchini Austria vijijini, wengi bado wanajenga nyumba za kitamaduni, ila zinaezekwa kwa tofali na wala sio nyasi ili kustahimili uzito wa theluji wakati wa majira ya baridi.
' Kwetu nyumba za kitamaduni mara nyingi zinajengwa kwa mbao ili kuhifadhi joto. Lakini paa ni sharti liwe imara. Wajua nchini Austria, tunashuhudia baridi kali sana.
Wakati wa theluji huwa ni matatizo makubwa. Sharti paa la nyumba liwe imara ili listahimili uzito wa theluji. Nyumba nyingi za kitamaduni zinaezekwa kwa tofali,'' anafafanua bwana Horst Stadler.
Ingawa kuna shinikizo la kiuchumi na kijamii kuachana na utamaduni wa kujenga nyumba za nyasi, inaonekana kwa wengine kama bwana Telewa, utamaduni huu bado utazidi kuendelezwa kwa gharama zote.
Comments
Post a Comment